DED MKOGA ASISITIZA WATOTO WENYE ULEMAVU WA NGOZI KUTOFICHWA
Posted on: August 21st, 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Dkt. Amon Mkoga amewataka wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kutofichwa nyumbani badara yake wapelekwe shuleni ili wapate elimu.
Ameyasema haya leo 21,Agosti 2025 wakati akizindua mradi wa BRIGHT FUTURE FOR CHILDREN WITH ALBINISM ambapo wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa ngozi, viongozi wa dini na wazee mashuhuri wameshiriki kujadiri namna bora ya kuwasaidia watoto hao kupitia mradi huo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo Mratibu wa mradi Ndugu Severine Mapunda amesema mradi unalenga kuwasaidia watoto wenye ulemavu kupata elimu na mahitaji muhimu ili waweze kuondokana na tatizo la kisaikolojia linalotokana na kutengwa na jamii
"inaonekana sehemu kubwa watoto wenye ulemavu wa ngozi wanakosa mahitaji muhimu huku watoto wengine wakitelekezwa na wazazi wao hii inapelekea wengi kupata msongo wa mawazo na kushindwa kufanya vizuri kwenye masomo yao" amesema Saverine
Naye Yusuph Bwango msimamizi wa mradi huo amesema mradi utaanza kwa kutoa elimu kwa wananchi ili kupunguza au kuondoa kabisa tabia ya kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu wa ngozi.amesisitiza kuwa kwa awamu ya kwanza mradi utafikia vijiji 22 na badae wataendelea na vijiji vingine.
Katika uzinduzi huo ameshiriki Afisa Elimu, Elimu Maalumu Mwalimu Chubwa ambaye amewasisitiza wazazi kupeleka watoto wenye ulemavu katika kituo cha Kakora Shule ya Msingi ambapo wataishi hapo na kupata Elimu huku ghalama zote zikitolewa na Serikali.
Wazazi wa watoto hao wamefurahia huduma zitakazotolewa na mradi huo na wameahidi kupeleka watoto hao shuleni kupata elimu.