Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imepandisha kiwango cha ufaulu wa elimu ya msingi hadi kufikia asilimia 93.44 na kufikia wastani wa ufaulu wa 203.61 ukilinganisha na mwaka 2024 ambapo ufaulu ulikuwa kwa asilimia 86.1% sawa na wastani wa ufaulu wa 177.24, mafanikio haya ni jitihada za pamoja za walimu, wanafunzi, uongozi wa Halmashauri pamoja na wadau mbalimbali wa elimu.
Akizungumza katika sherehe ya usiku wa Mwalimu katika ukumbi wa safari Club, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe.Ng’wilabuzu Ludigija, amewapongeza walimu wa shule za msingi kwa bidii na kujituma kwao, akisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na walimu
“Nawapongeza walimu wote wa Wilaya ya Kwimba kwa kazi kubwa na kujitoa kwenu katika kufundisha watoto wetu. Matokeo haya yanathibitisha kuwa bidii, nidhamu na ushirikiano huzaa matunda, Endeleeni kujituma zaidi ili kuongeza ufaulu na kuijenga kesho bora ya Taifa,” amesema Ludigija.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu ili kuwapa motisha na kuwezesha utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi wote.
Naye Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Dkt. Amon Mkoga, amesema ongezeko hilo limetokana na ushirikiano anaoutoa kwa walimu sambamba na utoaji wa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri katika masomo yao hususani masomo ya Hisabati na kiingereza
“Kuongezeka kwa ufaulu hadi kufikia asilimia 93.44 ni matokeo ya ushirikiano na uwajibikaji na huu ni mwanzo, nipende kuwaambia walimu nitaendelea kutoa ushirikiano pamoja na kuwapatia motisha walimu na shule zitakazo fanya vizuri lengo letu ni kufikia asilimia 96% ya ufaulu ifikapo mwaka 2026”amesema Mkoga
Mkoga ameongeza kuwa Halmashauri imeendelea kufanya vizuri katika upimaji wa kitaifa wa darasa la nne ambapo ufaulu umepanda hadi kufikia asilimia 87.14% huku lengo la halmashauri ni kufikia asilimia 98% ya ufaulu ifikapo 2026.
Walimu waliopongezwa wameahidi kwenda kuongeza juhudi ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka zaidi ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.