Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mh. Ng’wilabuzu Ludigija, ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa vibanda vya biashara unaoendelea katika stendi ya Zaman Ngudu, kwa lengo la kujiridhisha na hatua za utekelezaji wa mradi huo pamoja na ubora wa kazi zinazofanyika.
Akizungumza leo tarehe 7 januari wakati wa ziara , Mkuu wa Wilaya amesema mradi huo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza mapato ya Halmashauri na kutoa fulsa kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika maeneo rasmi na salama.
“matarajio ya Serikali ni kuona mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, ili vibanda hivyo viwanufaishe wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla” Amesema Ludigija
Mkuu wa Wilaya amewataka wakandarasi na wasimamizi wa mradi kuhakikisha wanazingatia ubora, muda wa utekelezaji na thamani ya fedha, huku akisisitiza ujenzi wa jengo la famasia uanze kutekelezwa mapema kwa kuzingatia ubora na viwango sahihi.
Kwa upande wao, wasimamizi wa mradi kutoka Halmashauri wamemueleza Mkuu wa Wilaya kuwa ujenzi unaendelea vizuri na wamejipanga kuhakikisha changamoto zozote zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati ili mradi huo ukamilike na kuanza kutumika kwa lengo lililokusudiwa.
Aidha Mkuu wa Wilaya amekagua utekelezaji wa ujenzi wa jengo la walinzi katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na ujenzi wa jengo la watoto njiti ambapo amewaelekeza wasimamizi wa miradi hiyo kukamilisha utekelezaji kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyotakiwa huku wakizingatia thamani ya fedha za miradi hiyo.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.