Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Mohamed Ngasinda, amewataka vijana wahitimu wa vyuo vya ufundi kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuchangamkia fursa zilizopo ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Akizungumza katika mahafali ya kwanza ya Chuo cha ufundi stadi(VETA)wilayani humo,Ngasinda alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana na wanawake kupitia programu za mafunzo ya ufundi na ujasiriamali zinazochangia kuwajengea uwezo, kuwapatia mtaji na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja pamoja na pato la taifa.
Ngasinda alisema jumla ya wahitimu 17 wamepatiwa mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa kupitia programu mbalimbali ikiwemo ya wanawake na Samia Scholarship, ambayo imelenga kuwainua wanawake kiuchumi kupitia kozi fupi za ufundi stadi.
“Wahitimu tayari mnazo fursa za kuzitumia katika soko la ajira. Nyinyi ni mafundi waliohitimu na mnaweza kuanzisha kampuni, miradi au vikundi vya ujasiriamali ili kujipatia kipato,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kwa kuweka mifumo ya kuwawezesha, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Katibu Tawala huyo aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata katika kujiajiri kupitia fursa za ufundi kama umeme, mabomba na ujenzi, pamoja na kufungua maduka ya vifaa vya ujenzi na miradi mingine ya uzalishaji.
Alisisitiza kuwa hakuna lengo la vijana kukaa kusubiri mikopo pekee, bali kutumia wataalam wa maendeleo ya jamii kupata ushauri sahihi wa kuanzisha miradi.
Ngasinda pia amewataka vijana kuendelea kulinda amani na kuepuka kudanganyika na makundi yenye misukumo mibaya.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na wahitimu 49 kutoka chuo cha Vefa, ambao wametakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kutumia ujuzi waliopata.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.