KIONGOZI MWENGE WA UHURU AIPONGEZA KWIMBA KUONGEZA WIGO UKUSANYAJI MAPATO
Posted on: August 28th, 2025
Mwenge wa Uhuru leo Agosti 28, 2025 umezindua vibanda vya biashara 20 pamoja na Jengo la Famasi katika soko la Ngudu wilayani Kwimba vilivyojengwa kwa thamani ya zaidi ya Milioni 168 kama mradi wa kudumu wa ukusanyaji mapato ya ndani.
Akizindua Mradi huo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 Bw. Ismail Ali Ussi amewapongeza Viongozi wa Wilaya hiyo kwa kubuni chanzo cha kudumu cha kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa halmashauri hiyo.
Amesema mradi huo una tija sana kwani kwa kupitia vyanzo kama Kodi za kupangisha, Leseni za biashara, Kodi za huduma kama Usafi na choo vitakua endelevu na kuisaidia halmashauri hiyo kukusanya fedha ambazo zitasaidia kuboresha mazingira ya soko hilo lakini pia kutekeleza miradi mingine ya huduma za jamii.
Amesema mradi huo ni miongozi mwa miradi inayoenda kuwapa hadhi Ngudu na halmashauri kwa ujumla na kuweza kupeleka hata kupandishwa hadhi kwa mji wa Ngudu hata kupata hadhi ya manispaa katika siku za usoni takribani mwaka mmoja ujao.
Akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Biashara wa Halmashauri hiyo Bi. Salome Mwaipopo amesema wameamua kujenga maduka hayo ili kukusanya mapato na kwamba kwa chanzo hicho pekee wamelenga kukusanya zaidi ya Tshs. Milioni 41 kwa mwaka.
Kadhalika, Kiongozi huyo ametoa wito kwa wananchi kujiandaa kushiriki katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 kwa amani na utulivu kwa ajili ya kupata viongozi wazuri kwa maendeleo yao.
Awali, Mwenge wa Uhuru umekagua huduma za matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na ujenzi wa bweni la wavulana katika shule ya Sekondari Ngudu vilivyogharimu zaidi ya Tshs. 175 kabla ya kutembelea mashine ya kuongeza virutubishi kwenye nafaka pamoja na mradi wa vijana washonaji.