MAMBO YA KUKIMBIZA SIMU KWA MTU AKUSOMEE MESEJI YAMEPITWA NA WAKATI
Posted on: August 14th, 2025
Haya yamesema na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija wakati akihutubia maadhimisho ya elimu ya watu wazima yaliyofanyika leo 14,Agosti 2025 katika viwanja vya Kwideko.
Mkuu huyo amewataka wananchi kupeleka vijana wao katika vyuo vilivyopo Wilayani Kwimba ambavyo ni Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malya, VETA, Chuo cha Michezo Malya na Chuo cha Afya Ngudu na Sumve.
Amesisitiza kuwa Serikali imepiga hatua katika kupambana na maadui watatu ukiwemo ujinga ambapo elimu inaendelea kutolewa " nimefurahi kuona wanawake watu wazima wako hapa wanajifunza kusoma na kuandika na kuhesabu hii elimu ya watu wazima inafaida sana, wito wangu tushirikiane kuhamasisha watu wapate elimu ili waondokane na ujinga na waachane na kusomewa meseji, mambo ya kukimbiza simu kwa mtu akusomee meseji yameshapitwa na wakati, jiungeni na elimu hii mpate maarifa" Ludigija
Amesisitiza kuwa ambao hawajuwi kusoma na kuandika wanapoteza haki zao hasa za kuchaguliwa kuwa viongozi kwani ili mtu awe kiongozi anapaswa ajue kusoma na kuandika.
Pia amewahamasisha wananchi kuwa tayari kushiriki uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 29,Oktoba 2025 ili wachague viongo bora watakao ongoza na kuhamasisha shughuli za maendeleo.
Katika maadhimisho hayo ameshiri Katibu Tawala Wilaya ya Kwimba Ndugu Mohamed Ngasinda ambaye amehamasisha Taasisi zote za Elimu kuhakikisha maadhimisho yajayo wanashiriki kikamilifu kuonyesha yale wanayofindishwa katika Taasisi zao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Dkt Amon Mkoga amewapongeza walimu wote wanaofundisha na amewahamasisha watu wote ambao hawakubahatika kupata elimu ya awali wajitokeze kujiunga kupata elimu ya watu wazima.
Akiwasilisha taarifa ya Elimu ya watu wazima Afisa Elimua ya Watu wazima Mwalimu Boniventure Ng'andiro amesema elimu ya watu wazima ni elimu inayotolewa kwa watu wazima waliokosa fulsa ya kupata elimu ya awali, amesisitiza kuwa katika kuboresha elimu ya watu wazima Serikali imeanzisha vyuo mbalimbali ikiwa ni pamoja na FDC, VETA na kuanzisha program mbalimbali shuleni ambapo watu wazima wanapata fulsa ya kujifunza na kupata ujuzi.