MKUU WA SHULE ASIYEONGEZA VIRUTUBISHO KWENYE CHAKULA ATACHULIWA HATUA
Posted on: August 1st, 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija amewataka watendaji kuhakikisha wanawasimamia walimu wakuu na Wakuu wa shule kusaga mahindi kwenye mashine zilizofungiwa mashine ya kuongeza virutubisho kwenye unga.
Ameyasema hayo 31,Julai 2025 wakati akifanya kikao cha tathmini ya lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri " Mkuu wa Shule asiyesaga unga kwenye mashine inayoongeza virutubisho tutamuondoa" Ludigija
Mkuu huyo amesisitiza kuwa virutubisho ni muhimu kwenye chakula cha wanafunzi ili kuzuia udumavu na athari nyingine za kiafya.
Aidha amewataka watendaji wa Kata na Wakuu wa Idara za Elimu kusimamia utoaji wa chakula chenye virutubisho, pia amewataka watendaji kuwachukulia hatua wazazi wote wasiowachangia chakula watoto wao hali inayopelekea watoto hao kuwa watoro
Mratibu wa lishe akiwasilisha taarifa ya lishe ya robo ya nne amesema asilimia 98 ya shule zote za Wilaya ya Kwimba zinatoa chakula kwa wanafunzi hivyo amesisitiza watendaji na Wakuu wa idara za elimu kuendelea kuhamasisha wazazi kuona umuhimu wa kuchangia chakula kwaajili ya watoto wao.
Naye mratibu wa Malaria amewashukuru Watendaji kwa ushirikiano wanaompatia pia amewashauri kuendelea kushirikiana katika zoezi la kunyunyizia viuwadudu vya Malaria ili kutokomeza Mbu waenezao gonjwa la Malaria.