MKUU WA WILAYA AHIMIZA USAWA WA KIJINSIA NA UWAJIBIKAJI
Posted on: March 6th, 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe Ng'wilabuzu Ludigija amewahimiza wananchi wote kutekeleza majukumu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, ameyasema hayo leo Machi 6,2025 katika maadhimisho ya siku ya wanawake ambayo kiwilaya yamefanyika Kata ya Sumve.
" niwapongeze wanawake mnaofanya kazi kama mlivyoonyesha hapo kazi zenu, tunatamani kuona wanawake wanafanya kazi za kiuchumi ndiyo maana Serikali inawapatia mikopo ili mfanye ujasiliamari muinuke kiuchumi"
Mkuu huyo amesisitiza kuwa Serikali inafanya juhudi kubwa za kumuinua mtoto wa kike kwa kuhakikisha anapata elimu bora kwa kuweka miundombinu wezeshi kama mabweni na hosteli ili waweze kusoma bila kupata changamoto zinazosababishwa na kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Aidha ametumia maadhimisho hayo kuwataka wanawake kupaza sauti pindi wanapoona watoto wa kike wanaozeshwa katika umri mdogo " kuweni mabalozi ukiona mtoto wako anaozeshwa katika umri mdogo kisa Baba anataka ng'ombe toa taarifa msikae kimya watoto hao wanahaki ya kusoma na kutimiza ndoto zao" amesema Ludigija
Katika maadhimisho hayo ameshiriki Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Dkt Amon Mkoga ambaye amewasisitiza wanawake kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kuondokana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Thereza Lusangija amewapongeza wanawake walioshiriki maadhimisho hayo na amewataka wanawake wote kuwa walinzi wa watoto wao kwa kuhakikisha watoto hawafanyiwi ukatili wa aina yoyote ile.
Akiongea kwa niaba ya Katibu wa CCM Wilaya Ndugu Ramadhan Omary amewashauri wanawake wote kujitokeza kugombea nafasi za uongozi
" wanawake wote kipindi hiki ni chakwenu, kupitia Rais tumewaamini kuwa mnaweza nafasi za uongozi,niwaombe wanawake mlioko hapa kipenga kikipigwa cha uchaguzi jitokezeni mkagombee nafasi mbalimbali"
Akisoma risala Bi. Lucia Malisa Afisa Maendeleo ya Jamii amesema maadhimisho ya wanawake yanafanyika kila mwaka Machi,8 ambapo kauli mbiu ya mwaka "wanawake na wasichana 2025 tuimarishe haki,usawa na uwezeshaji"