MKUU WA WILAYA ATOA MWEZI MMOJA KITUO CHA AFYA KIKUBIJI KIANZE KUTOA HUDUMA
Posted on: December 12th, 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija amewataka wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kikubiji kuhakikisha kituo kinaanza kutoa huduma kwa wananchi kabla ya Januari 18,2025.
Ameyasema hayo wakati akifanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo la Kwimba " kituo hiki kianze kutoa huduma za nje kwasababu jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Maabara yameshakamilika kwahiyo yatumike, Januari nikirudi hapa nikitu huduma zilishaanza kutolewa" Ludigija
Mkuu huyo amekagua majengo ya Kituo cha afya Hungumalwa ambapo ameelekeza jengo la upasuaji lianze kutoa huduma kwani vifaa vilivyokuwa vinakwamisha huduma hiyo vilishapatikana.
Aidha Mkuu wa Wilaya amekagua miradi ya elimu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa shule ya msingi Chasalawi ,Kiliwi, Buyogo na ujenzi wa shule shikizi Nyanhiga, pia amekagua ujenzi wa mabweni na madarasa Shule ya Sekondari Mihaya Cheyo na Bupamwa ambapo amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kuongeza kasi ya utekelezaji ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.
Akihitimisha ziara hiyo Mhe. Ludigija amewapongeza wananchi wa Kitongoji cha Mwasolwe Kijiji cha Nyanigha Kata ya Mwakilyambiti kwa kuanzisha ujenzi wa shule mpya kwaajili ya kuwasaidia wanafunzi kupata elimu karibu na makazi yao
" niwapongeze wananchi wote wa kitongoji hiki cha Mwasolwe mmefanya kazi nzuri ya kuanzisha shule lakini hata mlipopata fedha za kukamilisha mmesimamia vizuri majengo haya yanakaribia kukamilika hongereni sana" Ludigija
Naye Diwani wa Kata ya Mwakilyambiti Mhe. Deborah Lameck ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za kukamilisha madarasa ya shule hiyo iliyoanzishwa na Wananchi.
Wananchi waliokuwepo kwenye miradi hiyo wamemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta fedha za kutekeleza miradi Wilayani Kwimba na wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo.