Afisa Elimu Sekondari Mwalimu Emmanuel Katemi amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamilama kusoma kwa bidii na kuhakikisha matokeo ya mitihani ya Taifa ufaulu unaongezeka zaidi.
Ameyasema hayo leo Machi 21,2025 wakati akikagua utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ya kuwapatia motisha wanafunzi wa Shule hiyo kwa kuwapikia chakula ( wali na nyama ya kuku)
" kikubwa kilichowaleta hapa ni elimu kwahiyo niwatake msome sana tena kwa bidii ili ufaulu uongezeke zaidi, mnajua hii shule ni miongoni mwa shule bora hapa Tanzania kwa Shule za Serikali kwahiyo tunataka ufaulu uongezeke zaidi na mkifanya vizuri zaidi kwenye mitihani mtapata motisha nyingine nzuri zaidi" amesema Katemi
Aidha amewataka wanafunzi hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za shule hiyo ili kuwa na nidhamu nzuri, pia amewasisitiza kuzingatia elimu maana ndiyo lengo kubwa lililowapeleka shuleni.
Naye Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Japhet Sineno amemshukuru Mkurugenzi kwa kutoa motisha hiyo kwa wanafunzi kwani itakuwa chachu kwao kupenda masomo zaidi na kuongeza juhudi ili mitihani ijayo wafanye vizuri zaidi.
Nao wanafunzi wameishukuru Serikali kwa kutoa motisha ya chakula hicho na wameomba motisha za namna hiyo ziendelee kuwa zinatolewa pindi wanapofanya vizuri katika mitihani, wanafunzi hao wameahidi kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
Shule ya Sekondari Nyamilama imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya Taifa kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo jambo ambalo limewavutia wazazi wengi kupeleka wanafunzi katika Shule hiyo ambayo kwa sasa inawanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha tano, na zaidi ya wanafunzi 1300 wanakaa bweni na hosteli.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.