Kilio cha wakazi wa Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza cha kutaka mgawanyo wa Halmashauri mbili kinatarajia kutoweka, baada ya baraza la Madiwani la Halmashauri kuazimia kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, ili kupata Halmashauri mpya.
Wakizungumza katika kikao cha kuwasilisha mapendekezo ya ugawaji wa Halmashauri tarehe 19/02/2021 kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Madiwani wamesema wanayo shauku kubwa ya kupata Halmashauri mpya ili wananchi waweze kusogezewa huduma karibu na kuongeza chachu ya maendeleo.
Dhamira ya baraza la Madiwani la halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kupitisha pendekezo hilo, ni kutaka kuongeza chachu ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wilaya ya Kwimba na kusogeza karibu huduma kwa wananchi.
" Sisi hitaji letu ni kupata idhini ya kuanzisha Halmashauri mpya kwa vile vigezo tumetimiza tuombe hitaji letu lifanikiwe litakapofika ngazi za juu" amesema Peter Misalaba Diwani Kata ya Nyambiti.
Nae Mbunge wa Jimbo la Sumve Mhe.Kasalali Mageni amesema "Nawashukuru wote kuanzia Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi,Wakuu wa Idara na Madiwani kwa ushirikiano mnaoendelea kuuonyesha, ombi langu ushirikiano huu uendelee hadi tutimize hitaji letu la kupata Halmashauri mpya, tusikatishane tamaa,tusikwamishane njiani tushirikiane ili tutimize malengo ya kuwasogezea huduma wananchi ambalo ndiyo lengo la Raisi wetu Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli"
Baada ya mapendekezo hayo kupitishwa, kikao hicho kinatarajia kuyawasilisha katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Mwanza (RCC), ili kiweze kuweka baraka zake kisha itapelekewa kwenye Wizara husika, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( OR-TAMISEMI) ili nao waweke baraka kama wataridhishwa na vigezo vilivyoorodheshwa kwa ajili ya uanzishwaji wa Halmashauri mpya.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe.Senyi Simon Ngaga amewapongeza Waheshimiwa Madiwani kwa maamuzi hayo na amesisitiza kutokata tamaa pia ameshauri maandalizi ya kuongeza mapato ya ndani yaanze kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kiwango cha mapato kiongezeke zaidi.
Katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kwimba Bib.Pendo Malabeja ametoa taarifa na kuonyesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba inavyo vigezo vinavyozingatiwa katika ugawaji wa Halmashauri ikiwemo kigezo cha mapato ya ndani kufikia bilioni mbili,idadi ya wananchi inakidhi,Taasisi za muhimu yaani Afya,Elimu na nyingine zipo.
Mapendekezo ya uanzishwaji wa Halmashauri mpya yamepitishwa na Madiwani wote wa kata thelathini za Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na Madiwani kumi wa viti maalum walioridhia kuijenga Kwimba mpya.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.