Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Msafiri Simeoni ameuomba uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kutambua wajibu wake katika kutekeleza Mradi wa Mama na Mtoto (MnM) unaofadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia taasisi za “International Development Research Center” (IDRC) na “Global Affairs Canada” (GAC) na kutekelezwa kwa ushirikiano na kamati ya Afya Mkoa wa Mwanza na kamati ya Afya ya Wilaya ya Kwimba ili kusaidia vipaumbele vya Wilaya katika kuboresha afya ya mama na mtoto.
Mtemi aliyasema hayo wakati akijitambulisha kwa wajumbe wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa Mama na Mtoto kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo tarehe 23 Januari, 2018 katika ukumbi wa Ndilima Hoteli kata ya Hungumalwa Wilayani Kwimba.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon akijitambulisha kwa wajumbe wa kikao cha kuutambulisha Mradi wa Mama na Mtoto
Akiongea katika kikao hicho Mratibu wa Mifumo ya Afya Bibi Magdalena Mwaikambo kutoka Mradi wa Mama na Mtoto alisema
“ Mradi unawalenga akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano lengo likiwa ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kupitia uboreshaji na utoaji wa huduma muhimu za awali kwa mama mjamzito, wakina mama, watoto wachanga pamoja na watoto walio na umri chini ya miaka mitano na kuboresha namna ya utoaji wa huduma za afya pamoja na utumiaji wa huduma muhimu za makundi lengwa”.
Bibi Mwaikambo aliendelea kusema wameamua kufanya kazi Kwimba kwa sababu takwimu zinaonesha kuwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano viko juu ukilinganisha na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mwanza.
Mratibu wa Mifumo ya Afya Bibi Magdalena Mwaikambo akielezea Malengo ya Mradi.
Kwa upande wake Dr. Maendeleo Boniphance ( Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Bugando) chini ya Mradi wa Mama na Mtoto aliuomba uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kuhakikisha unasimamia zoezi kikamilifu ili kupata wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakaoweza kutekeleza majukumu yao katika jamii na Mradi utatoa mafunzo ya huduma jumuishi ya Mama na Mtoto kwa watoa huduma kwa kufuata mtaala wa wizara ya afya.
Akiendelea kuchangia Dr. Maendeleo alisema kuwa baada ya Mradi kukamilika tunatarajia kuongezeka kwa idadi ya akinamama wajawazito wanaojifungua katika vituo vya afya,kuboreka kwa mawasiliano kati ya watoa huduma katika vituo na jamii inayohudumiwa, kuboreka kwa miundombinu ya vituo katika utoaji wa huduma za afya, vituo kuwa na vifaa vyote muhimu kwa ajili ya huduma za afya ya uzazi na mtoto pamoja na kuimarika kwa viashiria vya utoaji huduma.
Dr. Maendeleo Boniphance ( Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Bugando) chini ya Mradi wa Mama na Mtoto akichangia Mada.
Kwa kuongezea Mwezeshaji kutoka Mradi wa Mama na Mtoto Anthony Mlila alisema Mradi utatoa mafunzo rejea jinsi ya kumhudumia mama mwenye dalili za kifafa/mwenye kifafa cha mimba, kutokwa damu nyingi baada ya kujifungu,kusaidia mtoto mchanga kupumua na kusambaza miongozo husika katika vituo vyote vya afya.
Aidha Afisa Mradi Ndg Leonard Masele alichangia kwa kusema Mradi huu utashirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya,Wakuu wa Idara na Vitengo,Kamati ya Afya ya Wilaya, Uongozi wa Kata,Kijiji,Kitongoji na jamii kwa ujumla.
Afisa Mradi Ndg Leonard Masele akielezea juu ya Ushirikishwaji wa Wadau mbalimbali katika kutekeleza Mradi
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Bibi Pendo A. Malabeja aliushukuru uongozi wa Mradi kwa kuleta mradi katika Halmashauri ya Kwimba na alisema uongozi wa Halmashauri ya Wilaya upo tayari kutekeleza Mradi kwa umakini na weledi wa hali juu na wananchi wategemee kupata huduma bora za afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Bibi Pendo A. Malabeja akitoa shukrani zake kwa wawakirishi wa Mradi.
Mradi huu umechukuliwa kutokana na ufaulu uliojionyesha katika kutekeleza mradi kama huu nchini Uganda kupitia Health Child Uganda (HCU) ambao ulifadhiliwa na Global Affairs (GAC) katika mradi wa MUSKOKA ambao ulitekelezwa kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbalala (MUST) mwak 2011 mpaka 2015 na kuonyesha matokeo chanya.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.