Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija ametoa wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka Kitengo maalumu cha ufuatiliaji na usimamizi wa dawa ya mifugo kama ilivyo kwa dawa za binadamu na vipodozi ili kuleta ufanisi katika uuzaji wa dawa za mifugo.
Mhe. Ludigija ametoa wito huo alipotembelea mabanda la Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na mabanda ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Agosti 06, 2024 katika viwanja vya Nyamhongolo yanapofanyika maonesho ya nanenane kwa Kanda ya Ziwa Magaharibi ambapo amewataka wataalamu hao kufikisha ujumbe huo katika ngazi ya juu wa ajili ya utekelezaji.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi ya wananchi kuhusu uuzwaji wa dawa za mifugo ambazo zimemaliza muda wake na hivyo kupelekea wananchi wengi kukosa imani na dawa hizo mwishowe kupoteza mifugo yao kutokana na magonjwa.
"Nimekutana na changamoto hii, wananchi wengi wanalalamika wanapewa dawa za kuosha ng'ombe ili kupe zife lakini hawaoni magonjwa hayo yakimalizika na Wataalamu wetu wamefatilia wamegundua dawa wanazouziwa wananchi hao ni feki na zingine zimekwisha muda wa matumizi".
Ni vizuri sasa wadau wetu wa mifugo kushirikiana na kuanza kufuatilia kwa karibu, kupita katika maduka hayo hata kwa kuanza na wale wasambazaji wakubwa ili tuweze kunusuru mifugo ya wafugaji inayokufa kila siku kutokana na kukosa dawa sahihi. Ameongeza Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha DC Ludigija amewapongeza wananchi wanaoendelea kutembelea maonesho hayo na kuwataka kutumia elimu ya kilimo wanayoipata kupitia maonesho hayo kujiletea mafanikio lakini pia amewataka wananchi hao kuwapatia pia elimu hiyo wale ambao hawakupata nafasi ya kutembelea maonesho hayo ili kuleta tija na mageuzi ya kilimo.
Mhe. Ludigija ametembelea maonesho hayo kujionea pia hali ya maandalizi ya kilele cha nanenane ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda na kutoa maelekezo kadhaa kwa waandaaji wa maonesho hayo ili kuboresha sherehe za kilele hicho.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.