DC LUDIGIJA AZITAKA TAASISI NA HALMASHAURI KUHAKIKISHA FEDHA ZA MIRADI ZINATEKELEZA MIRADI
Posted on: February 12th, 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe Ng'wilabuzu Ludigija amewataka viongozi wa Taasisi na Halmashauri kuhakikisha fedha zinazopokelewa kwaajili ya kutekeleza miradi zitumike kwa wakati na miradi ikamilike na kutoa huduma
" tunataka tuone fedha zilizoandikwa kwenye hizo karatasi mnazosoma zionekane kwa uhalisia kwenye miradi husika hatutaki maneno" amesema Ludigija
Haya yamejiri kwenye kikao cha ushauri cha Wilaya kilichofanyika leo Februari 12,2025 kikiwa na lengo la kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26.
Mheshimiwa Ludigija ametumia kikao hicho kuwataka maafisa maendeleo wa Kata kuvisaidia vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kuandaa maandiko na katiba za vikundi ili iwe rahisi kuomba mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri.
Pia amewataka watendaji wa Kata kuwakamata watu wote wanaokwamisha shughuli za elimu ikiwa ni pamoja na wazazi ambao watoto wao ni wanafunzi lakini bado hawajaripoti shuleni hasa wale wanaoanza kidato cha kwanza
"Kamateni watu wote ambao watoto wao bado hawajaripoti shuleni wawambie hao wanafunzi wako wapi na kama kuna viongozi wanaowakwamisha huko ngazi za vijiji nao wakamateni wakiwasumbua nipeni taarifa" amesema Ludigija
Katika kikao hicho bajeti za taasisi zilizopo Wilayani hapa zimejadiliwa zikionyesha vipaumbele vya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha taarifa ya Halmashauri Ndugu Yohana Muhandikila kwa niaba ya Mkurugenzi amesema kuwa katika mwaka 2025/26 Halmashauri imepanga kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu,afya na miradi ya utawala.
Naye Makam Mkuu wa Chuo cha Michezo Malya ndugu Denis Kayombo ametumia kikao hicho kuwakaribisha wanakwimba na wananchi wote kupeleka vijana kusoma katika chuo hicho bora kabisa na cha pekee Afrika Mashariki
" Chuo ni chetu kipo Wilayani kwetu na sasa hivi kuna mradi mkubwa wa bilioni 32 unaendelea ambapo inajengwa Akademi ya michezo ( sports academy) lakini wanakwimba hawapo, niwasihi muwalete vijana wasome michezo, siku hizi watu wanatajirika kupitia michezo " amesema Denis Kayombo