Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imetoa Jumla ya shilling 332,564,000/= Kwa wanufaika wa Mradi wa TASAF III. Lengo la mpango huo ni kuzisaidia Kaya Maskini 9263 kupata mahitaji ya msingi kama vile huduma za Elimu,Afya na kuongeza kipato katika familia.
Mratibu wa TASAF Wilaya ya Kwimba Ndg Barnabas Yawanga amewaomba wanufaika wa fedha za TASAF kuwa na matumizi sahihi .
“Hakikisheni Fedha mnazopata mnazitumia vizuri kwa ajili ya kumudu mahitaji ya msingi kama vile kuwapeleka watoto shule,kukata bima ya Afya,kumudu gharama za dharura katika familia, kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na kujiongezea kipato na hatimaye kuondokana na umaskini”
Kwa upande wake Mwezeshaji wa TASAF Ndg Matiku Magesa amewashauri walengwa wa Kata ya Nyambiti kuwa fedha wanayoipata wahakikishe wananunua chakula ili kupambana na makali ya bei ya chakula inayozidi kupanda wilayani kwimba.
Akitoa maoni yake Mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Nyambiti Ndg Richard Masele ameiomba Selikari iongeze kiwango cha fedha kwa Wanufaika wa Mradi kwani fedha wanayoipata ni kidogo ukilinganisha na hali halisi ya maisha.
Aidha Bibi Mariam Deus ambaye ni mnufaika wa kaya masikini katika kijiji cha Nyambiti amesema Fedha za Mradi wa TASAF zimemsaidia kujenga nyumba ya matofali na kuezeka kwa bati.
Akionyesha msisitizo namna Mradi unavyomnufaisha, Mzee William Musa amesema fedha anazozipata humsaidia kununua chakula pamoja na mahitaji madogomadogo ya familia anayoiongoza.
Mradi wa TASAF awamu ya III umereta manufaa makubwa kwa wananchi waliokuwa na hali duni ya maisha na hivyo kuchochochea maendeleo endelevu miongoni mwa kaya hizo pamoja na jamii ambayo siyo wanufaika wa Mradi.Wananchi wa Kwimba wanatoa pongezi na shukrani nyingi kwa Serikali kwa namna inavyowahudumia.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba
30 Mei 2017.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.