Wajumbe wa Kamati ya fedha,Uongozi na Mipango wawapongeza viongozi wa Kijiji cha Hungumalwa kwa maamuzi ya kujenga Shule ya Sekondari ya Kijiji chao, Wananchi wamezoea kujenga Shule za kata lakini katika Kijiji hiki imekuwa tofauti kwani wananchi wameamua kujenga Shule ya Kijiji chao baada ya kuona wanafunzi wao wanatembea umbali mrefu kwenda Sekondari ya Kata iliko.Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 09 Agosti,2021 huko Hungumalwa wakati Kamati hiyo ikifanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha Shule hiyo imefunguliwa mwaka huu ambapo wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaendelea na masomo katika madarasa matano yaliyokamilika huku wananchi wakiendelea na ujenzi wa madarasa mengine matano ambayo kwa sasa yamefikia hatua ya boma. Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Theleza Lusangija amewapongeza kwa hatua hiyo na amewashauri kuendeleza ushirikiano huo wenye tija kwa wananchi.
Katika ziara hiyo miradi ya Elimu na Afya imetembelewa ambapo katika Shule ya Sekondari Walla Maabara tatu zimekaguliwa na ukarabati wa Maabara hizo uko katika hatua za ukamilishaji huku milioni 42.7 zikiwa zimetumika kutoka Serikali kuu na nguvu za Wananchi.
Aidha Kamati hiyo imekagua ujenzi wa madarasa mawili na Ofisi katika Shule ya Msingi Igunguhya ambapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ameshauliwa kusimamia kwa umakini shughuli zinazofanyika katika eneo lake la kazi ikiwemo ujenzi.
Kamati hiyo imekagua ujenzi wa Zahanati ya Sangu ambayo iko katika hatua za ukamilishaji huku milioni 79.8 zikiwa zimetumika kutoka Serikali kuu, Halmashauri na nguvu za Wananchi.Hapa kamati imeshauri ujenzi huo ukamilike haraka ili huduma zianze kutolewa mahali hapo.
Vilevile Kamati hiyo haikuishia hapo imeweza kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba inayojengwa eneo la Icheja kata ya Ngudu.Hapa kamati imepongeza wasimamizi wa ujenzi huo kwa hatua iliyofikiwa ambapo majengo zaidi ya kumi yakiwa yamekamilika na mengine machache yako kwenye hatua ya ukamilishaji.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.