Wilaya ya Kwimba imeadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kupanda miti 1010 katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la Icheja linakojengwa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.
Awali kabla ya kupanda miti wananchi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija wamefanya mazoezi ya viungo katika uwanja ya Kwideco na kisha wamekimbia umbali wa kilomita 4 kuelekea eneo la kupanda miti.
Akiongea na wananchi baada ya mazoezi hayo Mkuu wa Wilaya amewataka Wananchi kuuenzi Muungano kwa kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi wa Taifa,pia amewasisitiza watenge muda wa kufanya mazoezi ili kujenga afya bora.
Aidha Mheshimiwa Ludigija amewataka Wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kujiepusha na athari za mabadiriko ya tabia ya nchi.
Katika maadhimisho hayo ameshiriki Katibu Tawala Wilaya ya Kwimba Ndug. Mohamed Ngasinda ambaye amewasisitiza watumishi wote kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano huku wakizingatia umoja ulioanzishwa na Waasisi wa Taifa hili.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Dkt. Amon Mkoga amewasisitiza watumishi kutenga muda wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujikinga na magonjwa nyemelezi.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza miaka 61 tangu kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, kauli mbiu ya mwaka huu inasisitiza wananchi kuendelea kuuenzi Muungano na kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 " Muungano wetu ni dhamana,heshima na tunu ya Taifa,shiriki uchaguzi mkuu mwaka 2025"
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.