Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imeadhimisha siku ya mtoto wa Afrika katika kijiji cha Isageng’he kata ya Mwakilyambiti tarehe 16/06/2017 Kauli mbiu ikiwa “Maendeleo Endelevu 2030 Imarisha Ulinzi na Fursa sawa kwa watoto” lengo la maadhimisho hayo ni kuwakumbuka watoto wenzetu waliouawa na utawala dharimu wa makaburu wa Afrika ya kusini tarehe 16.06.1976, katika kitongoji cha Soweto.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya kwimba Ndg Joseph Mwikwabe ambaye ni Afisa Tarafa ya Nyamilama amewaomba wazazi/walezi wa watoto na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na fursa sawa kwa watoto wote bila ubaguzi.
“Tunapambana vikali ili kutokomeza kabisa ubaguzi wa watoto katika kupatiwa elimu kikamilifu na ndoa za utotoni kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaohusika kuoa au kuwapa mimba wasichana wadogo”.
Ndg Joseph pia ameagiza kuwa viongozi wote katika vitongoji,vijiji, kata na wilaya wahakikishe amani inakuwepo miongoni mwa watoto na wazazi/walezi ili kudhibiti mimba kwa wasichana kitu ambacho inabidi tukikemee kwa nguvu zetu zote. Hii ni pamoja na kuweka/kuwepo miundo mbinu rafiki shuleni na hasa kwa watoto wenye ulemavu na wanafunzi wote kwa ujumla.
Akisoma Risala kwa Mgeni Rasmi Mtoto Salumu Jonas Lutaja kwa niaba ya watoto wa wilaya ya kwimba ameiomba jamii kutekeleza Haki za Msingi za Watoto ikiwa ni pamoja na Haki ya kuishi, Haki ya kulindwa, Haki ya kupata elimu bora na Haki ya kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Ndg Joseph kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ametoa Zawadi ya Vyandarua kwa akina mama watano (05) wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao walikuwa wanaoudhuria cliniki vizuri ili ziweze kuwasaidia na kuwakinga watoto hao na ugonjwa wa Malaria.
Aidha Meneja wa Bank ya CRDB Tawi la Ngudu Bibi Elizabeth Lucas amewafungulia watoto hao watano akaunti ya watoto “Junior Jumbo Account” katika bank ya CRDB Tawi Ngudu na kwa gharama ya shilling elfu tano tano kila mmoja.
Kwa kuhitimisha sherehe hizo Ndg Joseph ametoa shukrani zake kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na vikundi vya kijamii na wadau wote kwa jitihada zao za kuwasaidia watoto walio katika mazingira hatarishi. Mchango wao tunauthamini na tunaomba tuzidi kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya wilaya yetu ili tuweze kusaidia watoto wengi zaidi.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.