Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe Ng'wilabuzu Ludigija amewapongeza viongozi na wasimamizi wa elimu wa Halmashauri ya Kwimba kwa kupandisha ufaulu kwa kiwango kikubwa.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 13,2024 kwenye baraza la Madiwani robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/24 ambapo taarifa ya matokeo ya kidato cha sita imeonyesha kuwa Shule ya kwanza, ya pili na ya tatu kimkoa zimetoka Wilaya ya Kwimba huku Shule ya Sekondari Tallo ikiwa nafasi ya saba Kitaifa kati ya Shule zaidi ya 929
" kazi iliyofanyika ni kubwa sana niwapongeze viongozi wote kwa usimamizi pia niwapongeze walimu kwa kutimiza wajibu wao, walimu hao waliosababisha kwimba itambulike wapewe motisha ili waendelee kufanya vizuri zaidi" amesema Ludigija
Mheshimiwa Ludigija ametumia wasaa huo kuwataka madiwani kwenda kusimamia elimu huku wakisisitizwa kushirikiana na Walimu kuzuia utoro wa wanafunzi ili kuendelaa kupandisha ufaulu.Pia amewataka waheshimiwa Madiwani kwenda kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kwimba Ndugu Aziza Isimbula ametumia wasaa huo kuwashauri Madiwani kwenda kufanya mikutano ya kuwaeleza wananchi miradi inayotekelezwa na Serikali pia ameipongeza Halmashauri kwa kuweza kukusanya mapato ya ndani zaidi ya asilimia 100 ya lengo hali iliyopelekea fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya robo mwaka Bi. Happiness Msanga Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Elimu, hali inayoongeza hamasa ya wanafunzi kupenda masomo na kufanya vizuri kwenye mitihani.
Madiwani walioshiriki Mkutano huo wamempongeza Mkurugenzi na wataalamu wote wanaosimamia elimu kwa kupandisha ufaulu " shule ni zilezile na walimu niwalewale lakini ni miaka mitatu mfululizo matokeo yanakuwa mazuri sana kwakweli tunampongeza Mkurugenzi kwa usimamizi mzuri, tuwaombe walimu na wataalamu wote wasirudi nyuma tena wasonge mbele zaidi matokeo yajayo tuwe wakwanza kitaifa" amesema Mhe. Gervas Kitwala
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.