Watendaji wa kata wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba wametakiwa kuhakikisha wanasaidia kukomesha tabia za utoro shuleni. Wanafunzi wanaoandikishwa shule sharti wamalize shule na wanakuwapo Shuleni kila siku za shule, watoro wote wapewe adhabu kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu za shule.
Wito huo umetolewa na Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza ndugu, Juma Kasandiko wakati wa kikao cha Mpango mkakati wa kuinua Taaluma Mkoa wa Mwanza kilichofanyika wilayani Kwimba katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Ngudu na baadaye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Nella. Kikao hicho kiliwashirikisha Wakuu wa Shule,Walimu Wakuu, Watendaji wa Kata, Waratibu Elimu Kata na Walimu wa Taaluma.
Katika kikao hicho Ndugu Juma Kasandiko aliwataka Walimu kujisomea zaidi ya vitabu vitatu ili wawe na maarifa ya kutosha na kutumia njia shirikishi wakati wa ufundishaji na ujifunzaji. Pia amewakumbusha wakuu wa shule kuteua wakuu wa Idara za Masomo wenye maarifa ya kutosha katika masomo hayo. “Suala hili litatufanya kufikia mpango mkakati tuliojiwekea wa kupata daraja la kwanza kwa asilimia 50 la pili asilimia 40 na la tatu asilimia 10”, alisisitiza.
Aliendelea kumpongeza Mkuu wa Shule wa Shule ya Sekondari Mwamashimba Bi. Edina Mkama kwa kufaulisha vizuri mtihani wa “MOCK” kidato cha sita mwaka 2017.Katika matokeo hayo, idadi ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni wanafunzi 86, daraja la pili wanafunzi 02 na jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 88.
Afisa Elimu huyo wa Mkoa amewaomba Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kuwashirikisha Walimu wao katika shughuli zote zinazofanyika Shuleni ili kuondoa mpasuko wa wao kwa wao na amewataka kuitisha vikao vya mara kwa mara ili kupeana taarifa mbalimbali juu ya boreshaji wa elimu.
Afisa Elimu Taaluma Sekondari Mkoa wa Mwanza Ndugu, Joseph Ngoseki aliwaonya Wakuu wa Shule wenye upendeleo wa kuwapa motisha walimu kwani kwa kufanya hivyo ni kuwawakatisha tamaa walimu katika kutimiza wajibu na majukumu yao. “Wakuu wa Shule na Walimu wa Wakuu hakikisheni mnawapongeza walimu wanaofanya vizuri”.
Aidha alikemea vitendo viovu vinavyofanywa na Walimu wa kiume kwa kuwakatisha masomo watoto wa kike na ameahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu watakaokutwa na makosa hayo.
Wakatiwa kufunga kikao hiyo Afisa elimu sekondari Bw Lawi Kajanja alimuunga mkono Bw Joseph Ngoseki kwa kuwatahadharisha walimu na umma kwa ujumla kuwa ni kosa kisheria kusababisha au kushawishi mwanafunzi kutohudhuria masomo yake kwa namna yoyote ile. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Na.25 ya Mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 2013 sehemu ya 35, ibara ya 4 (sehemu ndogo ya ii-iii) ya kifungu hicho.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.