“ Madereva mnatakiwa kutunza magari mliyokabidhiwa na serikali kwa manufaa ya umma na kuwa mawakili wa vyombo mlivyopewa” hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya wilaya ya Kwimba Bibi Pendo Anangisye Malabeja wakati wa kikao kazi cha kuwakumbusha majukumu madereva kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba.
Aidha alisisitiza kuwa dereva wa umma anaongozwa na kanuni sheria na taratibu hivyo anaweza kupangiwa kufanya kazi katika idara za Serikali ilimradi asikiuke kanuni na taratibu za Serikali na amewakumbusha umuhimu wa kutunza nyaraka za Serikali.
Alisisitiza kuwa ni marufuku dereva kunywa pombe wakati wa kazi na watakaobainika wakiwa wamelewa wakati wa kazi hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa kuunga mkono maelekezo ya Mkurugenzi Mtendaji Afisa Utumishi bibi Christina Bunini, aliwaagiza Madereva wote kuhakikisha kuwa magari wanayoendesha yana Nembo inayoitambulisha gari kuwa ni ya Halmashauri ya wilaya Kwimba.
Mweka hazina wa wilaya Bw, Emmanuel Masele alisema Madereva wanatakiwa kufuata sheria za usalama barabarani, kujaza ‘logbook’ wawapo safarini na kuhakikisha zinasainiwa na Mkuu wa msafara pia aliwakumbusha kufunga mikanda wawapo safarini kwani ni kwa ajili ya usalama na pia matakwa ya kisheria.
Mkaguzi wa Ndani wilaya Ndugu Maro Kenyunko alitoa ushauri kwa Afisa usafirishaji wa Halmashauri kuhakikisha anahakiki leseni za madereva wote kama ziko hai na kuhakikisha magari ya Halmashauri yanapaki saa 12.00 jioni.
Mhandisi wa Ujenzi wa wilaya Ndugu Makongoro Igungu alimuomba mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kufufua Karakana ili wataalam wa magari waliopo waweze kutumika na kuipunguzia Halmashauri mzigo mzito wa kupeleka matengenezo magari kwa wazabuni wakati ina wataalam wanaoweza kurekebisha baadhi ya matatizo kwenye magari.
Akihitimisha kikao kazi hicho, Bibi Pendo aliwasisitiza madereva kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.