Mbio maaalum za Mwenge wa Uhuru zinazokimbizwa na Luteni Josephine Paul Mwambashi Mkimbiza Mwenge Kitaifa akiwa na timu ya wakimbiza mwenge sita zimefika Wilaya ya Kwimba leo tarehe 9 Julai 2021 na kukimbia Km 100.4, kukagua,kuzindua na kuweka Jiwe la Msingi kwenye miradi 11 yenye dhamani ya bilioni 1.5.
Akiongea katika maeneo mbalimbali Luteni Josephine Paul Mwambashi amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kwa kusimamia vizuri fedha za Serikali kitu kilichopelekea miradi yote kukubarika na kupitishwa na Mwenge.
Katika mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Hungumalwa Luteni Josephine amewapongeza Wananchi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kujenga Shule katika kijiji cha Hungumalwa ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa nane kwenda Shuleni.
Aidha Luteni Josephine amewataka viongozi kuwa makini katika utunzaji wa nyaraka mbalimbali zinazokuwepo kwenye utekelezaji wa miradi ya Serikali ili kuonyesha uwazi wa hatua zinazokuwa zikifanyika katika miradi.
Katika kijiji cha Mahiga Luteni Josephine amepongeza juhudi za kuwasogezea wananchi huduma ya maji kwani ujenzi wa tanki umewezesha kaya zaidi ya 4000 kupata maji safi na salama, ambapo amewashauri RUWASA kuongeza mtandao wa maji kutokana na uhitaji wa Wananchi.
Akizindua jengo la Baba, Mama na Mtoto katika Hospitali ya Ngudu Luteni Josephine amewashukuru wafadhili ( Aghakan) waliojenga jengo hilo kwani kuwepo kwa jengo hilo kumeboresha huduma za Afya hasa kwa mama wajawazito na watoto kwani vifo vya wazazi vimepungua kwa kiwango kikubwa.
Mkimbiza Mwenge huyo amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona kwani ugonjwa huo upo. " Niwaombe wananchi wote muendelee kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona kwa kunawa mikono na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa wakati wote.Atakayekuwa hana barakoa huyo hatapaswa kuongozana na sisi katika Mwenge huu" amesema Luteni Josephine.
Katika Mbio hizo jumbe mbalimbali za Mwenge zimesomwa ikiwemo ujumbe wa Malaria,ujumbe wa kupinga rushwa,ujumbe wa Ukimwi,ujumbe walishe,ujumbe wa dawa za kulenya pamoja na ujumbe wa TEHAMA uliokuwa umebeba kauli mbiu ya Mwenge isemayo "TEHAMA ni Msingi wa Taifa endelevu,itumie kwa usahihi na uwajibikaji"
Wakimbiza mwenge hao wakisoma jumbe hizo katika maeneo mbalimbali wamewasisitiza wananchi kutumia teknolojia ya Habari na mawasiliano katika mambo mazuri kama kusoma kwa njia ya mtandao, kufanya biashara, kuangalia taarifa mbalimbali zinazotokea siyo kuutumia teknolojia kufanya uhalifu.
Mwenge huo umeondoka Wilaya ya Kwimba na kuelekea Mkoa wa Shinyanga ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ameukabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ukiwaka na kung'ara.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.