Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mheshimiwa Ng'wilabuzu Ludigija amewataka Wananchi wenye tabia za kuwanyanyasa wajane hasa kuwanyang'anya mashamba na mali nyingine waache tabia hiyo.
Ameyasema hayo leo Septemba 25,2023 wakati wa ziara yake ya kusikiliza malalamiko na kero za Wananchi iliyofanyika katika Kata ya Kikubiji na Bupamwa
"acheni tabia ya kuchukua mali za wajane na watoto wao kwa kisingizio cha mali za ndugu yenu, hizo mali ni za mjane na watoto wake nyie ndugu wengine tafuteni mali zenu" Ludigija
Mkuu huyo amewataka viongozi wa vijiji na Kata kuhakikisha wanatatua migogoro ya Ardhi ambayo imeonekana kuwa kero kwa wananchi wengi hasa wanaogombania mashamba ya familia.
Aidha Mheshimiwa Ludigija amewaelekeza wananchi wote waliovamia eneo la Kituo cha Afya Kikubiji kuondoka eneo hilo na kuacha kufanya shughuli za kilimo
"kuanzia leo ni marufuku kufanya shughuli zote kwenye eneo la Kituo cha Afya Kikubiji, Mahakama ilishaamua kesi kwahiyo atakayelima au kufanya kazi yoyote tutamchukulia hatua za kisheria' Ludigija
Mkuu huyo amewataka RUWASA kuweka utaratibu mzuri wa upatikanaji wa maji Ili kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu kutafuta Maji
" niwaelekeze RUWASA mpange ratiba ya upatikanaji wa maji hata kama kwa wiki itakuwa mara moja au mara mbili lakini Kila kata ijue maji yanatoka siku gani na iwe mchana siyo usiku"
Wananchi walioshiriki ziara hiyo wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuona umuhimu wa kusikiliza kero na malalamiko na kuyatatua.
Mkuu wa Wilaya ataendelea na ziara hiyo ya kusikiliza malalamiko na kero za wananchi ambapo kesho atakuwa Kata ya Nyamilama na Hungumalwa.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.