Mradi wa Mama na Mtoto ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Canada kwa kishirikiana na Chuo Kikuu cha Calgary pamoja na Chuo Kikuu cha Afya cha Katoliki (CUHAS-Bugando) Mwanza.Lengo kuu la mradi ni kuboresha utoaji wa huduma za muhimu za awali kwa mama mjamzito, wakina mama, watoto wachanga pamoja na watoto walio na umri chini ya miaka mitano na kuboresha namna ya utoaji huduma za afya pamoja na utumiaji wa huduma muhimu za makundi lengwa Wilayani Kwimba.
Akizungumza katika zoezi la tathimini ya vifaa tiba na vitendea kazi katika hospital, Zahanati na Vituo vya afya wilayani Kwimba Dr. Dismas Matovelo Msimamizi wa mradi wa Mama na Mtoto amesema shughuli za Mradi huo ni pamoja na utekelezaji wa uboreshaji huduma kwa kuzingatia matokeo ikiwemo ukarabati wamiundombinu ya vituo (Majengo,Umeme,, Maji) na ununuzi wa vitendea kazi na vifaa tiba,kujengea uwezo timu za Halmashauri na kamati za vituo katika usimamizi na uendeshaji wa utoaji huduma za afya na kutoa mafunzo, kusimamia na kufuatilia watoa huduma wa afya wa jamii na kufanya kazi na makundi ya jamiiili kukuza na kuboresha namna ya utoaji wa huduma za afya.
Dr. Maendeleo Boniphance ( Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Bugando) chini ya Mradi wa Mama na Mtoto akikagua Kitanda cha kujifungulia katika Zahanati ya Kiliwi.
Naye Bibi Magdalena Mwaikambo Mwezeshaji kutoka Mradi wa Mama na Mtoto aliwaomba wajumbe wa Kamati ya Afya ya Wilaya kuhakikisha wanashiriki na kusimamia kwa Uthabiti Mradi wa Mama na Mtoto ili uweze kuleta mafanikio chanya kwa walengwa waliokusudiwa. Aliyasema hayo wakati akiutambulisha Mradi kwa wajumbe wa Kamati ya Afya ya Wilaya 'CHMT"
Bibi Magdalena Mwaikambo Mwezeshaji kutoka Mradi wa Mama na Mtoto akiutambulisha Mradi kwa Kamati ya Afya ya Wilaya ya Kwimba.
Kwa upande wake Bibi Tumsifu Matutu mwezeshaji kutoka kutoka Mradi wa Mama na Mtoto alisema mradi utaziwezesha kamati za Afya, vituo vya kutolea huduma kufanya usimamizi shirikishi na ushauri katika kuboresha huduma vituoni ilikuboresha ubora wa takwimu na utoaji wa huduma.
Bibi Tumsifu Matutu mwezeshaji kutoka Mradi wa Mama na Mtoto akielezea Masuala ya usimamizi shirikishi.
Akichangia DR. Rose Mjawa Laiser kutoka katika Mradi wa Mama na Mtoto alisema ili Mradi uweze kufanikiwa suala la Usawa wa Kijinsia lazima lizingatiwea Sehemu za kutolea huduma za Afya.
DR. Rose Mjawa Laiser kutoka katika Mradi wa Mama na Mtoto akielezea Masuala ya Usawa wa Kijinsia mahali pa kutolea huduma
Akihitimisha ziara, Dr. Mtengwa D.M kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba iko tayari kufanya kazi na Mradi wa Mama na Mtoto kwakuwa takwimu zinaonesha kuwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano viko juu ukilinganisha na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mwanza.
Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ina jumla ya hospitali 1 ya wilaya, vituo vya Afya 5 na Zahanati 44 zinazotarajia kunufaika na Mradi wa Mama na Mtoto.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.