Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bwana Thobias Makoba amewataka Maafisa Habari wa serikali Mkoani Mwanza kubuni habari mpya za kimkakati zenye kuitangaza miradi ya maendeleo ya serikali.
Bwana Makoba ameyasema hayo leo tarehe 19, Julai 2024 wakati alipokua akizungumza na Maafisa Mawasiliano kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa, Taasisi, Mashirika na Makampuni mbalimbali ya serikali Mkoa wa Mwanza katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
"Na hapa Mwanza ninajua kuna miradi mbalimbali ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya SGR hivyo tusisubiri ijitokeze dosari ukimbilie kutoa taarifa ya ufafanuzi , ni wakati sasa wa kubadili namna ya utoaji wa taarifa zetu". Amesisitiza Makoba.
Aidha, amesema umekua ni utaratibu wake kukutana na Maafisa Mawasiliano kila mahali aendapo lengo likiwa ni kujitambulisha lakini pia kusikiliza na kuchukua maoni, mawazo na mapendekezo mbalimbali ambayo yatasaidia kuboresha utendaji kazi.
"Kuwa msemaji mkuu sio kwamba unajua kila kitu, tunategemeana katika kuhabarisha kwani serikali ni moja, " amefafanua Makoba.
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amesema Mkoa wa Mwanza ni Mkoa wa kimkakati kwa kuwa ndio lango kuu kwa kanda ya ziwa na ndio kitovu cha uchumi hivyo Maafisa Habari wanategemewa kwenye uhabarishaji na serikali inawapa ushirikiano mzuri.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (RS Mwanza) Bw. Paulo Zahoro amesema hali ya uhabarishaji kwa Mkoa wa Mwanza ni nzuri hata kufikia hatua ya kushinda nafasi ya pili na kupata Kikombe na Cheti cha Ushindi kutoka kwa Waziri wa Habari Mhe. Nape Nnauye kwenye Kongamano la Habari lililofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Juni mwaka huu.
Maafisa Mawasiliano nao wamemshukuru Msemaji Mkuu wa Serikali kwa kutambua umuhimu wao na wameahidi kutekeleza maelekezo waliyopewa.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.