Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amemtaka Mkandarasi Kwiyera Interprises Limited kukamilisha ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kufikia Disemba 30,2023 ili awamu zingine za ujenzi ziendelee na kuwapatia watumishi na wananchi huduma nzuri.
Ametoa agizo hilo mapema leo akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo kwenye wilaya ya Kwimba alipotembelea ujenzi huo unaofanyika kwenye kata ya Ngudu kwa zaidi ya Bilioni 4 ambapo bilioni 1.3 zitatumika kwa awamu ya kwanza.
"Mkandarasi leo umechelewa na umeshaongezewa mara nne muda wa kukamilisha nami kwa kuzingatia ucheleweshaji wa malipo ya fedha kwa mkandarasi huyo nakutaka sasa ukamilishe jengo hili hadi disemba 30 mwaka huu."
Aidha, Makalla amemshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha zaidi ya Bilioni 4 kwa ajili ya Ujenzi wa jengo hilo (Bilioni 1.3 awamu ya kwanza) ambapo amebainisha kuwa litasaidia kuwaweka watumishi kwenye mazingira nadhifu ya kufanyia kazi na wananchi kupata huduma nzuri.
Awali Mkuu wa Wilaya ya kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija alifafanua kuwa Mkandarasi huyo amekua na mwenendo wa kusuasua kwenye ujenzi hadi kufikia hatua ya kuongezewa muda kwa mara tatu baada ya muda wa awali kuisha kwa mujibu wa mkataba pamoja na kupatiwa fedha.
Akikagua hali ya utoaji huduma kwenye Hospitali ya Wilaya iliyojengwa kwa zaidi ya Bilioni 4 kwenye eneo la Icheja kuanzia mwaka 2018/19 CPA Makalla amewapongeza Kwimba kwa kukamilisha ujenzi ambapo wagonjwa zaidi ya 475 wanalazwa kwa mwezi na kusaidia mtiririko wa huduma.
"Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za ujenzi na vifaa vya kisasa, tunatambua kazi nzuri inayofanywa na wataalamu wa afya ila lazima tusimamie matumizi ya lugha nzuri kwa wagonjwa kwani inaleta matumaini hata kabla ya kuanza kutoa huduma yenyewe" Amesisitiza CPA Makalla.
Akitoa taarifa ya Ujenzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Happness Msanga amebainisha kuwa fedha hizo zilitoka kwa ajili ya ukarabati wa iliyokua hospitali ya wilaya eneo la kakora lakini kutokana na ufinyu wa eneo waliamua kujenga hospitali mpya.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.