Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba umefanya ziara ya kutembelea kituo cha Afya cha kutolea huduma Kahangala kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Magu pamoja na kituo cha afya cha kutolea huduma Karume kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela tarehe 6 Januari, 2018 lengo likiwa ni kupata uzoefu wa matumizi ya Fedha zilizotumwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya ukarabati au ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya.
Akiongea katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Ndg Lutengano George Mwalwiba, aliushauri Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kuhakikisha unafuta muongozo uliotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi hiyo ikiwa ni pamoja na matumizi ya “ Force Account” ili kupunguza gharama na kuongeza ubora wa majengo.
Ndg Mwalwiba aliendele kusema ni vizuri kumshirikisha Mganga Mkuu wa Mkoa katika hatua zote ili kuepusha mkanganyiko katika utekelezaji wa Mradi.
Kwa upande wake Ndg Joel Ally mjumbe wa kamati ya Afya katika Zahanati ya Kahangala alisema kamati ya Afya ndiyo moyo wa mradi wajumbe wanatakiwa kujitoa na kuwa na moyo wa kujituma ili mradi uweze kutekelezeka katika hali ya ubora na viwango vilivyokusudiwa.
Akiendelea kuchangia Ndg Mwalwiba alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kuhakikisha anawandikia barua za uteuzi wasimamizi wa Mradi ili kila mtu atakayezembea awajibishwe katika eneo lake.
Baadhi ya Majengo ya kutolea huduma katika kituo cha Afya Kahangala Wilayani Magu
Kwa kuongezea Ndg Mwalwiba alisema pamoja na ujenzi wa Wodi ya akinamama, Maabara, Chumba cha kuhifadhia maiti, Jengo la Upasuaji, Matundu Manne ya choo na ujenzi wa Nyumba moja ya Mtumishi. Pia Halmashauri ya Wilaya ya Magu imejipanga kufanya ukarabati katika nyumba za watumishi .
Wodi ya kinamama kaika kituo cha Afya Karume Manispaa ya Ilemela
Akizungumza katika Ofisi yake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela Ndg John Paul Wanga alieleza jinsi matumizi ya “Force Accont” yalivyoleta Manufaa makubwa katika utekelezaji wa Ujenzi wa kituo cha Afya Kanyerere.
“Force Account imetupa manufaa makubwa ni pamoja na kupata majengo imara kwa kutumia mafundi watu, tumetengeneza ajira kwa wananchi na kazi imekamilika kwa wakati”
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela Ndg John Paul Wanga akiongea na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon amewapongeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili kwa moyo wa kujitolea katika kutekeleza miradi ya serikali na amewaomba wasichoke pindi wataalamu wa ujenzi watakapokuja kujifunza kwa awamu ya pili.
Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imepokea kiasi cha Shillingi Millioni Mianne 400,000,000/= kwa ajili ya kutekeleza Ukarabati au Ujenzi wa Kituo cha Afya Malya ikiwa ni lengo la Serikali la kutekeleza mkakati wa kuviboresha na kujenga vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili viweze kutoa huduma bora inayoendana na mahitaji halisi ya wananchi.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.