Viongozi wa vijiji na vitongoji watakiwa kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa wakati wote wa kazi ya sensa.Haya ameyasema Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Johari Samizi leo tarehe 15,Agosti 2022 wakati akiongea na watendaji na wenyeviti wa vijiji na vitongoji vya Kata ya Sumve na Mantare.
Elimu ya Sensa imeendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ya Wananchi wakiwemo viongozi wa vijiji na vitongoji ambapo ushirikiano baina ya viongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji wamesisitizwa kutoa ushirikiano kwa makarani watakaofanya kazi ya sensa ya watu na makazi.
“toeni ushirikiano kwa makarani, viongozi msiposhiriki kikamilifu kutoa taarifa sahihi kwa makarani mtakuwa mmewatendea dhambi kubwa wananchi kwa sababu takwimu zisipokuwa sahihi mtawasababisha wananchi wakose huduma muhimu kama dawa, maji, umeme, barabara na huduma nyingine nyingi hivyo sensa ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu mnatakiwa kushiriki kikamilifu” amesema Samizi
Aidha Diwani wa kata ya Sumve Mhe. Kitwala ameitumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa vijiji na vitongoji kuwa tayari kushirikiana na makarani wa sensa ili kuhakikisha takwimu zitakazopatikana zinakuwa sahihi ili maendeleo yaweze kuwafikia katika kata hiyo kulingana na uhitaji uliopo
“ niwaombe viongozi wenzangu mfanye kazi, waandaeni watu wetu kuwa tayari kuhesabiwa ili tupate takwimu zitakazosaidia kupanga mikakati ya maendelo, naamini watu wetu wako tayari kuhesabiwa tuendelee kuwahamasisha ili ikifika siku ya sensa watoe ushirikiano wa kutosha” amesema Kitwala
Sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka kumi,hivyo mwaka huu sensa inatarajiwa kufanyika tarehe 23,Agosti 2022 ambapo kila mwananchi atahesabiwa.”Sensa kwa maendeleo jiandae kuhesabiwa”
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.