Wenyeviti wa Serikali ya vijiji wametakiwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi na umakini wa hali ya juu ili kukamilisha miradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Haya yamejiri katika kikaokazi cha wenyeviti wa vijiji kilichofanyika leo tarehe 11, Oktoba 2022 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Ngudu. Katika kikao hicho viongozi hao wa vijiji wamepata maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna bora ya kufanya kazi kwa kuzingatia mipaka na wajibu wa kiongozi.
Aidha katika kikao hicho taatifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo imewasilishwa na Afisa Mipango Ndugu Rogatevane John Kipigapasi huku akisisitiza ushirikiano wa viongozi wa vijiji katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa kwenye vijiji vyao inatekelezwa na kukamilika kwa wakati.Afisa huyo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imepokea zaidi ya bilioni nne kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa madarasa 112 katika Shule za Sekondari ambayo yataghalimu bilioni 2.24
“ niwaombe viongozi wa vijiji mkasimamie mradi huu wa madarasa kwani yanatakiwa kukamilika kabla ya Disemba 15 kwahiyo bila usimamizi mzuri na waushirikiano hatutaweza, hivyo tushirikiane kusimamia, kila mtu afanye kazi kwa nafasi yake” amesema Kipigapasi
Afisa mipango akiwasilisha taarifa hiyo amewataka viongozi wa vijiji kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa ushuru wa mazao pale inapobidi kulipa amesema kutorosha mazao ni makosa makubwa yanayoisababishia Halmashauri ishindwe kukusanya fedha zinazoweza kuongeza maendeleo katika Wilaya ya Kwimba.
Pia amewasisitiza viongozi hao kwenda kutoa Elimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa kukopa mkopo usio na riba wa Halmashauri,” Halmashauri inatarajia kukopesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavi zaidi ya milioni 200 kwahiyo waambieni vijana waunde vikundi waje wapewe mikopo wakafanye kazi zakuwaongezea kipato” amesema Kipigapasi
Katika kikao hicho ameshiriki Afisa Kilimo Magreth Kavalo ambaye ametoa elimu ya kilimo na maandalizi ya mashamba kwaajili ya msimu wa wakilimo unaoanza sasa “ kulingana na utabiri wa hali ya hewa mvua haitakiwa nyingi kama mwaka jana kwahiyo naomba muwaambie wananchi waandae mashamba mapema, wawe tayari kulima mazao ya aina zote yakiwemo yale yanayostahimili ukame,vilevile niwaombe wakulima ambao bado hawajasajiliwa wafanye usajili ili wapate urahisi wa kupata mbolea kwa bei nafuu ukilinganisha na bei iliyoko sokoni mfano mbolea inauzwa 136,000 lakini mkulima aliyesajiliwa anauziwa kwa 70,000” amesema Mhandisi Kavalo
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Ndugu Denis Kabogo akihitimisha kikao hicho ametoa ufafanuzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiwasisitiza viongozi hao kwenda kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika vijiji vyao . Pia amewataka viongozi hao kwenda kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora katika kila kaya “ kahamasisheni ujenzi wa vyoo bora kwa kila Kaya na muwaambie wananchi ukaguzi utafanyika watakaokutwa hawajajenga Choo bora watatakiwa kulipa faini ambayo itaanzia 50,000 na kuendelea” amesema Kabogo
Wenyeviti walioshiriki kikao hicho wameushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kuona umuhimu wa kufanya kikao na wameomba vikao vya namna hiyo vifanyike marakwamara ili wapate nafasi ya kuwasilishwa hoja zao kwa viongozi.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.