Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Johari Mussa Samizi amewataka wadau wa zao la Pamba kuhakikisha wanazingatia taratibu za ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima. Ameyasema hayo leo tarehe 24,Mei 2022 kwenye kikao cha Wadau ambao ni Vyama vya msingi vya ushirika(Amcos),Kampuni za ununuzi wa Pamba na Maafisa Ugani na Viongozi wengine, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Ngudu.
" kila mtu ale kwa jasho lake, tuache wakulima wanufaike na jasho lao hata kama tuliwawezesha kwa mbegu na vitu vingine lakini bado wao ndio wanaotoka jasho mashambani" amesema Samizi
Mkuu huyo amewasisitiza wadau hao kuwa katika msimu huu wa Pamba uuzaji utafanyika kwa kutumia Amcos na Kampuni hivyo Kijiji kimoja kitakuwa na madirisha yaani vituo vya kuuzia pamba zaidi ya kimoja hivyo Mkulima atachagua aende kuuza kituo gani ambacho kitakua na bei inayomridhisha.Aidha Mhe. Samizi amesisitiza kuwa mtu yeyote atakayegundulika kununua kinyume na taratibu hatua kari za kisheria zitachukuliwa.
Katika kikao hicho Amcos wamesisitizwa kutunza kumbukumbu sahihi ili wakulima wapate mapato yatakayotokana na pamba iliyoletwa. Pia amewasisitiza kuhakikisha wakati wa ununuzi wa Pamba mizani yote itakayotumika iwe sahihi " Mizani isichezewe, nasisitiza muache tabia ya kuchezea mizani ili muwaibie wakulima atakayegundulika atafungwa" amesema Samizi
Naye Afisa Kilimo wa Wilaya ya Kwimba Mhandis Magreth Kavalo amewaelekeza wadau hao majukumu yao wakati wa ununuzi wa Pamba, pia amesasisitiza kufanya ushindani wa bei ili kila mfanyabiashara anunue pamba kulingana na uwezo wake " tunachokitaka ni ushindani wa bei, hakuna kuchagua mtu wa kufanyanae biashara ila bei ndiyo itamfanya Mkulima alete Pamba" amesema Kavalo
Wadau wa pamba wametangaziwa bei ya Pamba iliyoko sokoni kwa sasa ambayo ilitangazwa rasmi na Serikali kuwa ni Shilingi 1560 kwa kilo moja ya Pamba, Hivyo Mkulima hatakiwi kuuza pamba chini ya bei hiyo.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.