Wakuu wa Mikoa nane inayojishughulisha na kilimo cha Pamba ambayo ni Geita, Kagera, Kigoma, Singida, Simiyu, Shinyanga, Tabora na Mwanza wamefanya ziara Wilayani Kwimba kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kufufua zao la pamba ambalo kwa takribani miaka mitano uzalishaji wake umeshuka.
Akisoma taarifa kwa Wakuu wa Mikoa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon alisema Wilaya ya Kwimba imenufaika kupitia kilimo cha pamba cha mkataba kwa kuwapatiwa pembejeo za mkopo, uwezeshwaji wa huduma za ugani kutoka kwa makampuni na uundaji wa vikundi vya wakulima (FBGs).
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kilimo cha Pamba kinachangamoto ya Upungufu wa mvua uliosababisha wakulima wengi kushindwa kupanda mbegu za pamba na wengine ambao walikuwa wameshapanda kurudia tena kutokana na mbegu walizopanda mara ya kwanza kutoota kabisa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. John .V.K.Mongella, alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Mhandisi Mtemi Msafiri Simeoni kwa kusimia vizuri mikakati iliyotumika kufanikisha Kilimo cha Mkataba Wilayani Kwimba wakati ya ziara ya utembelea shamba la pamba la Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama(W) na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba. Aliendelea kusema kuwa, Wilaya ya kwimba ndiyo Wilaya kinara kwa Mkoa wa Mwanza kwa kulima pamba, hivyo amempongeza sana Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon kwa mchango wake wa hali na mali wa kufanikisha kilimo cha pamba Wilayani Kwimba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa singida Dkt.Rehema Nchimbi aliongezea kwa kumuomba Mkuu wa wilaya ya Kwimba awapatie vibarua wanaovuna pamba vifaa vya kuzuia vumbi ili kuepukana na vumbi kuingia kwenye njia ya hewa kwani bila kufanya hivyo vibarua hao afya zao zitakuwa hatarini.
Naye Ndg Bulugu Furano ambaye ni mkulima wa zao la pamba katika kijiji cha Isunga alisema pamba yake imeshambuliwa na wadudu aina ya ‘thrips’ na kusababisha pamba kunyauka na kudondosha majani na vitumba ambavyo havijakomaa, hivyo ameiomba Serikali kuhakikisha inapiga marufuku usambazaji wa dawa bandia kwa wakulima. Mkulima mwingine Ndg Buruma Nzobe aliongezea kwa kuiomba Serikali kupanga na kutangaza bei itakayomnufaisha mkulima kwani mpaka sasa bado Serikali haijatangaza rasmi bei ya pamba itakayotumika katika msimu huu.
Akitoa maelezo ya kuhitimisha ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanri amewaomba wakulima wa pamba wazalishe pamba safi na amesisitiza kuwa hakuna mtu atakaeuza wala kununua Pamba chafu.
Tokea miaka ya 1980 Wilaya ya Kwimba ilikuwa miongoni mwa Wilaya za kuigwa katika kanda ya ziwa kwa uzalishaji wa zao la pamba ikufuatiwa na Wilaya ya Maswa.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.