Wananchi wa kijiji cha Kadashi Kata ya Maligisu wameahidi kujitolea mali na nguvu ili kufanikisha uanzishwaji wa ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi.
Ahadi hizi zimetolewa leo tarehe 25,Julai 2022 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kati ya Wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe Johari Samizi, mkutano uliolenga kuwahamasisha Wananchi kujitokeza kushiriki ujenzi wa madarasa unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 1,Agosti 2022.
Akiongea katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya amewaeleza Wananchi kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingi katika kijiji hicho ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya uliofikia hatua za ukamilishaji na miradi mingine, amesisitiza kuwa ujenzi wa madarasa utasaidia wananfunzi wa Shule ya msingi kusoma katika mazingira mazuri bila msongamano darasani.
Aidha Mheshimiwa Samizi ameutumia mkutano huo kuwataka Wananchi kuhifadhi chakula ili kujiepusha na hatari ya njaa inayoweza kujitokeza.
" tunakoelekea tunakwenda kwenye njaa ya ajabu kwa sababu mmevuna chakula kingi lakini mnakiuza chote, nawaeleke kila familia kuhakikisha mnatunza chakula cha akiba msiuze mazao yote, mtapata njaa na hakuna chakula cha msaada" amesema Samizi
Mheshimiwa Samizi ameutumia mkutano huo kutoa elimu ya umuhimu wa sensa, amewataka wananchi waliohudhulia mkutano huo kuwa mabalozi kwa watu wengine kuhamasisha watu wote kujitokeza kuhesabiwa tarehe 23, Agosti 2022. Amesema kuwa kupatikana kwa idadi kamili ya Wananchi waliopo katika kila eneo kutarahisishia Serikali kutoa huduma sahihi kwa watu sahihi.
" Serikali ikiwa na takwimu sahihi za idadi ya watu wanaoishi kila eneo mfano Kadashi italeta wahudumu wa Afya kulingana na wingi wa watu, itatengeneza miundombinu na vitu vingine kulingana na uhitaji, hivyo niwaombe mjitokeze kuhesabiwa na msiwafiche walemavu nao wanahaki ya kuhesabiwa" amesema Samizi
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.