Umekuwa utaratibu wa baadhi ya watu wanaoishi maeneo ya vijijini kujenga nyumba na kuzipaua kwa bati bila kupigilia misumari ili kushikiza bati na mbao badara yake mawe ndio yanawekwa juu ya bati, jambo hili limeonekana kuwa ni hatari hasa pindi mvua za upepo zitakaponyesha mawe hayo yanaweza kusababisha majanga.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mheshimiwa Ng'wilabuzu Ludigija amewataka Wananchi ambao wamejenga nyumba na kuziwekea mawe juu ya bati, kuondoa mawe hayo na mabati yapigiliwe misumari Ili kujiepusha na majanga yanayoweza kuzuirika
" niwaombe Wananchi wenye nyumba za (slop) imarisheni nyumba zenu, tumieni misumari badara ya mawe maana tumeshaambiwa mvua za mwaka huu zitakuwa kubwa huenda zikawa na upepo unaoweza kusababisha hayo mawe yakawaangukia waliolala ndani" amesema Ludigija
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo leo Oktoba 9,2023 wakati akisikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Bugando na Iseni.
Aidha Mheshimiwa Ludigija amewasisitiza wananchi wa Kata ya Bugando kuhamasisha watoto wao kupenda Shule kwani Kata hiyo imeonekana kuwa na changamoto ya utoro hasa kwa wanafunzi wa Sekondari
"wazazi wahamasisheni watoto kwenda Shule waache utoro, tambueni kuwa Elimu ndiyo urithi pekee utakaomsaidia mtoto wako siyo mashamba ambayo yanasababisha migogoro ya ardhi kila siku" Ludigija
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ametatua changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji,umeme, migogoro ya Ardhi pia amewahamasisha wazazi kuchangia vyakula ili wanafunzi wapate chakula shuleni.
Naye Diwani wa Kata ya Bugando Mheshimiwa Chenyenge ameitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za kutekeleza miradi ya Elimu, maji na Barabara.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.