Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Mhe. George Simbachawene ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kusimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa Miradi ya zaidi ya Bilioni 100.5 inayotekelezwa na Mpango wa TASAF kwenye Mkoa huo ili iwe bora na ikamilike kwa wakati.
Mhe. Simbachawene ametoa agizo hilo leo tarehe 03 Agosti, 2023 wakati akikagua Ujenzi wa Majengo ya Jengo la Maabara, Wodi ya Wazazi na Upasuaji yanayotekelezwa kwa zaidi ya Milioni 291.8 zilizotolewa na Serikali kuu chini ya mpango wa TASAF huku zikitarajiwa kuwanufaisha zaidi ya Wananchi Elfu 72 kutoka kwenye kata tano.
"Lengo la miradi ya TASAF ni kupambana na umasikini na kuboresha maisha ya watanzania, moja kati ya maeneo yanayonyong'onyeza ni mwananchi kukosa matibabu anapougua ila sasa hapa Serikali imeonesha nia ya kuboresha maisha ya mtanzania" Mhe. Simbachawene.
Mhe. Waziri amefafanua kuwa kila mmoja ana wajibu wa kusimamia ujenzi na utekelezaji wa mirad ya TASAF kama miradi mingine inavyofanywa kwani fedha hizo zinatolewa mahsusi kuwahudumia wananchi kuwaondoka kwenye adha mbalimbali kama Miundombinu ya barabara, Afya, Elimu na mingine.
"Hongereni kwa kujenga kituo kizuri cha Afya, suala la kupata gari la wagonjwa kwenye kituo hiki haliepukiki hivyo niwaahidi tu kuwa nitalifanyia kazi ombi la Mhe. Diwani ili muweze kupata gari la wagonjwa kwenye kituo hiki." Amefanua Mhe. Waziri wakati akijibu ombi la Diwani wa kata hiyo.
Aidha ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Kwimba kwa kuanzisha ujenzi wa kituo cha afya kwa kutumia Mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo ya zaidi ya Milioni 300 zilizopelekwa hapo kujenga Jengo la Wagonjwa wa nje, Wodi za wanaume na wanawake pamoja na Miundombinu ya choo.
"Kwa ninavyofahamu uendashaji wa Halmashauri, ni lazima maamuzi haya yamewatia kwenye lawama sana maana watumishi wengi wanatamani fedha za mapato ya ndani zinaenda kutumika kwa kulipana posho ila nyie mliamua kuleta mradi huu wa muhimu kwa wananchi." Amefafanua Simbachawene.
Vilevile, ametoa siku 30 kwa TASAF Makao Makuu kwa kushirikiana na TAKUKURU kufuatilia kwenye Mitandao ya simu ili kubaini kiasi na sababu ya upotevu wa fedha zilizohaulishwa kwa wananchi masikini kupitia mitandao ya simu na kusababisha kutowafikia walengwa na hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija ametumia wasaa huo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapatia zaidi ya Bilioni 1.5 kujenga Miundombinu ndani ya Wilaya chini ya mfuko wa huduma za Jamii na amewapongeza wananchi kwa kuchangia nguvu kazi kwenye ujenzi.
"Miradi hii imekua na manufaa makubwa kutokana na kwamba inakwenda kuwagusa wananchi moja kwa moja na kwakweli tunampongeza Mhe. Rais kwa kutuletea fedha kupitia mradi wa Kunusuru Kaya Masikini kwani ameonesha nia ya dhati ya kuwasaidia wananchi kupitia huduma za jamii", Amefafanua Mhe. Mkuu wa Wilaya.
Naye Ndugu John Steven, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TASAF Makao Makuu amefafanua kuwa pamoja na miradi mbalimbali ya Ujenzi wa Miundombinu zaidi ya wanufaika Elfu 11 wanapata uhaulishaji wa fedha za kuwanufaisha kujikimu na kwamba kwa mkoa wa Mwanza kuna wanufaika zaidi ya elfu 71.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi kuhakikisha kamati za ujenzi za vijiji zinahusika moja kwa moja kwenye utekelezaji wa Miundombinu na akatoa wito kusimamia kwa karibu na kuongeza kasi ili ujenzi uweze kukamilika kwa wakati na huduma zianze kutolewa kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi.
Akiwasilisha taarifa ya Ujenzi wa Mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Ndugu Emanuel Lameck ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Sumve amefafanua kuwa majengo hayo Matatu kwa pamoja yanatekelezwa kwa zaidi ya Milioni 291 kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii chini ya mpango wa Kunusuru Kaya Masikini.
Naye Mhe. Gelfasi Kitwala , Diwani kata ya Sumve amewasilisha ombi kwa Mhe. Waziri la kupatiwa msaada wa Garii la kubeba wagonjwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi zaidi ya Eldu 72 wa Tarafa ya Ngulla.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.