Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Bi. Happiness Msanga amewaelekeza watendaji wa Kata na Vijiji kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato kwa uaminifu.
Ameyaelekeza hayo leo tarehe 11,Novemba 2022 kwenye kikao cha Robo ya kwanza ya mwaka cha Watendaji wa kata na vijiji kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Ngudu
“ukusanyaji wa mapato siyo jambo la hiari, ni takwa la kisheria kwahiyo iwe jua iwe mvua lazima tukusanye mapato” amesema Msanga
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa ukusanyaji wa mapato ni jukumu la watumishi wote hasa watendaji wa vijiji na kata japo kuna baadhi ya watendaji ambao hawatimizi wajibu huo.
Aidha amekemea baadhi ya watendaji ambao siyo waaminifu katika kukatia ushuru “ baadhi yenu siyo waaminifu mnaungana na wafanyabiashara kudanganya takwimu za mazao mnayokatia ushuru acheni tabia hiyo mara moja na tunaendelea kutafiti tutakayemkamata tutamchukulia hatua za kisheria”
Katika kikao hicho watendaji wameelekezwa kuhamasisha lishe bora hasa kwa watoto na wanawake wajawazito “hakikisheni lishe bora inakuwa agenda ya kudumu kwenye mikutano yenu, tena naelekeza shule zote ziwe na shamba la viazi lishe au mahindi lishe na mbogamboga ili wanafunzi wapate chakula shuleni”amesema Johari Samizi Mkuu wa Wilaya ya Kwimba
Akiwasilisha taarifa ya lishe Ya robo Mratibu wa Lishe Emma Kalolo ameeleza athari za ukosefu wa lishe bora kuwa ni watoto kuzaliwa wakiwa na mdomo sungura, kichwa kikubwa, tumbo kubwa na magonjwa mengine na udumavu.
Watendaji walioshiriki kikao hicho wameahidi kwenda kutekeleza maagizo hayo ikiwa ni pamoja na kuibua mikakati mingine ya kuongeza ukusanyaji wa mapato
“ maelekezo tumeyapokea, tutaongeza juhudi katika kukusanya mapato ikiwa ni pamoja na kuibua vyanzo vipya na kusimamia vyanzo vilivyopo” amesema Salum M.Salum Mtendaji wa Kata ya Hungumalwa
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.