Naibu waziri wa Nishati na Madini DKT. Medard M.Kalemani amezindua Mradi kabambe wa Umeme Vijijini REA awamu ya tatu Mkoani Mwanza tarehe 13 Julai 2017. Uzinduzi huo Kimkoa Umefanyika katika kijiji cha Nyamatala kata ya Ngulla Wilayani Kwimba.
Tumelenga kuwaunganishia wateja 720,515 katika mkoa wa Mwanza tunaomba wananchi wa Mkoa wa Mwanza waanze kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao. Hayo yamesemwa na Meneja wa TANESCO Kanda ya Ziwa Mhandisi Amos Maganga wakati akiongea na wananchi wa kijiji cha Nyamatala.
Naye Naibu waziri wa Nishati na Madini DKT. Medard M.Kalemani amesema Mradi huu wa umeme vijijini hauna Chama wala Dini na utawekwa kwenye kila nyumba hivyo basi vijiji na vitongoji vyote vya Mkoa wa Mwanza vilivyoachwa na Mradi wa REA awamu ya pili vitawekewa Umeme bila kusahau Taasisi za Umma ambazo ni Vituo vya Afya, Zahanati,Makanisa ,Misikiti,Shule pamoja na Mitambo ya Maji.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini DKT Medard M.Kalemani akiongea na wananchi wa Kijiji cha Nyamatala Wilayani Kwimba wakati wa Uzinduzi wa Umeme Vijijini REA awamu ya tatu.
Mkoa wa Mwanza umeunganishwa na umeme Mkubwa wenye nguvu ya 400kb, Mhe Naibu Waziri DKT. Medard amewaomba wananchi waanze kujenga viwanda vidogovidogo,viwanda vya kati na viwanda vikubwa kwa ajili ya kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Mkoa wa Mwanza una jumla ya vijiji mia tatu arobaini na tatu (343) ambavyo havijapata umeme hivyo basi vijiji 174 vya Mkoa wa Mwanza vinakwenda kupata umeme ndani ya miezi ishirini na nne (24) kuanzia sasa na vitakamilika mwezi Aprili 2019 na vijiji mia moja sitini na tisa (169) vilivyobaki vitapata umeme kuanzia mwaka 2019 na kumalizika mwaka 2020/2021. Mhe. Naibu Waziri DKT. Medard ameyasema hayo wakati wa kumtambulisha na kumkabidhi Mkandarasi NIPO GROUP Kampuni ya kizalendo ya kitanzania ambayo itafanya kazi ya uwekaji wa umeme Vijijini REA awamu ya tatu.
Aidha ametoa maelekezo mbalimbali kwa kampuni ya kizalendo NIPO GROUP kuhakikisha inaajiri wakandarasi katika maeneo watakayokuwa wanafanya kazi.
“Kwimba,Sumve Ngudu na maeneo mengine tunataka wakandarasi wazalendo wa maeneo hayo wapate ajira”
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mwanza Bibi Sarah Assey(kulia) akiwa na Kampuni ya kizalendo NIPO GROUP
Amemuagiza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mwanza Bibi Sarah Assey kuhakikisha anafungua ofisi ndogo za umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza.
“Meneja wa TANESCO fungua ofisi ndogo ya Umeme Nyamatara,Hungumalwa, Sumve na maeneo yote yenye mkusanyiko wa watu weka muhudumu wa TANESCO Kwa ajili ya kuhudumia wateja”
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongela ametoa maelekezo kwa wakuu wa Wilaya wote na Wakurugenzi wa halmashauri wote kuwa kila mwezi apate taarifa Mkoani ya utekelezaji wa Mradi wa REA awamu ya tatu.Pia amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya.
“Hakuna mtanzania mwenye akili timamu wala asiye mtanzania asiyeona kazi anazozifanya tunamuombea sana Mwenyezi Mungu amzidishie ampe afya ya mwili na akili ili aweze kutupeleka kwenye nchi ya Maziwa na Asali”
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongera Akitoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wakati wa Sherehe za Uzinduzi wa Umeme Vijijini awamu ya tatu.
Ngudu-Kwimba
Sanduku la Posta: P.O.BOX 88
Namba ya Simu: 0732 980528
Simu ya Kiganjani: 0732980528
Barua Pepe: ded@kwimbadc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.